Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Botswana Duma Gideon Boko wametangaza kuinua ngazi ya uhusiano wa nchi hizo mbili na kuwa ushirikiano wa kimkakati wa kina.
Hayo yamejiri wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika jana Jumanne hapa mjini Beijing. Akibainisha kuwa mwaka huu ni wa maadhimisho ya miaka 105 tangu kuasisiwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China na miaka 60 ya uhuru wa Botswana, Xi amesema vyama tawala vya nchi hizo mbili vinapaswa kuimarisha ushirikiano na kufanya mawasiliano ya kina kuhusu uzoefu wa utawala.
Rais Xi ameongeza kuwa China inaiunga mkono Botswana katika kufuata njia ya maendeleo inayolingana na hali halisi ya nchi hiyo. Alizitaka pande zote mbili kuboresha zaidi mfumo wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, na kutumia fursa mpya zinazotokana na sera ya China ya ushuru sifuri kwa bidhaa kutoka nchi za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China.
Amebainisha kuwa China iko tayari kuimarisha ushirikiano na Botswana katika nyanja za uchumi wa kidijitali, kilimo, ufugaji na sekta nyinginezo, pamoja na kutekeleza mradi wa elimu janja.
