Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ameridhia marekebisho ya katiba yanayoondoa hitaji la katiba ya kudumu na mwafaka wa kitaifa kukamilika kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
Bunge la Mpito la Kitaifa la Sudan Kusini lilipitisha marekebisho hayo Septema Mosi, na rais Kiir kuridhia siku inayofuata Septemba 2.
Marekebisho hayo yanatenganisha uchaguzi wa Desemba 22 na mchakato unaoendelea wa kuandaa katiba na mpango wa kufanya sensa ya watu na makazi, ambavyo vyote vimeorodheshwa kama masharti ya uchaguzi chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2018.
Sudan Kusini imeahirisha uchaguzi mara kadhaa tangu ipate uhuru wake mwaka 2011.
