Umoja wa Afrika (AU) umekaribisha kupitishwa kwa azimio la ‘Ramani Sahihi’ ya Afrika na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Azimio hilo linalenga kushughulikia upotoshaji ulioundwa na makadirio ya Mercator, mfumo wa uchoraji ramani wa karne ya 16 uliotengenezwa hasa kwa ajili ya usafiri wa majini. Makadirio haya yanafanya maeneo yaliyo karibu na ncha kuonekana makubwa zaidi huku yakipunguza ukubwa wa maeneo yanayozunguka Ikweta.
Umoja wa Afrika umesema azimio hilo ni zaidi ya uchoraji ramani, kwani linasisitiza umuhimu wa kuiwakilisha Afrika kulingana na hali halisi ya kijiografia iliyothibitishwa kisayansi.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Bw. Mahmoud Ali Youssouf ameitaja hatua kuwa ni muhimu kuelekea uwakilishi sahihi zaidi wa Afrika na maeneo mengine ya dunia. Aliipongeza Togo kwa kutetea mpango huo kwa niaba ya Kundi la Afrika na amemshukuru Rais Faure Essozimna Gnassingbé wa Togo kwa uongozi wake katika kuhamasisha suala hilo.
