Waziri wa Afya wa Tanzania, Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania itaendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje na kuimarisha usalama wa afya nchini na barani Afrika.
Mchengerwa amesema hayo jana jijini New York, Marekani, katika kikao kilichoandaliwa na Serikali ya Sierra Leone, kando ya kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 81), unaofanyika New York, alipoiwakilisha Tanzania katika mjadala kuhusu namna ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana Sierra Leone katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuongeza huduma za chanjo.
Mchengerwa amesema Tanzania inaunga mkono kikamilifu Mpango wa Utetezi wa Umoja wa Afrika (AU Champion Roadmap) wa mwaka 2026–2030, unaolenga kufikia malengo ya ‘Zero Tatu’, ikiwemo kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani usio na wataalamu, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga pamoja na kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.
