
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bi. Mao Ning amesema, hivi karibuni mabalozi maalum na mjumbe maalum wa China wamefanya ziara katika nchi saba za Mashariki ya Kati, Kanda ya Ghuba na Pembe ya Afrika, zikiwa ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia za China katika kupunguza mivutano na kukomesha uhasama.
Bi. Mao amesema, mjumbe maalum wa serikali ya China anayeshughulikia mambo ya Mashariki ya Kati Balozi Zhai Jun, mjumbe maalum wa mambo ya Afrika wa serikali ya China Balozi Liu Xianfa na mjumbe maalum anayeshughulikia mambo ya Pembe ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Balozi Hu Changchun, walikuwa kwenye ujumbe huo.
Katika ziara hizo mabalozi maalum na mjumbe maalum wamekutana na viongozi wa nchi husika, mawaziri wa mambo ya nje na maofisa wengine wanaoshughulikia mambo ya nje na usalama wa taifa. Bi. Mao ameongeza kuwa wamefanya mazungumzo kuhusu kuimarisha uhusiano wa pande mbili, huku wakibadilishana maoni kwa kina na pande zote kuhusu kuhimiza kupunguza mivutano ya kikanda na kufikia maelewano kadhaa ya pamoja juu ya kuimarisha mshikamano na ushirikiano, kulinda amani na kukuza maendeleo.