Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetoa ripoti mpya kuhusu hali ya Sudan likisema, wakimbizi zaidi ya milioni 5.145 wa Sudan wamerejea makwao, lakini mpaka sasa bado kuna watu milioni 8.6 ambao wamekosa makazi.
Ripoti hiyo imeonesha kuwa, wakimbizi hao wamerejea kufuatia kuboreka kwa hali ya usalama katika baadhi ya sehemu za Sudan, ambao asilimia 82 kati yao walikuwa ni wakimbizi wa ndani nchini Sudan na wengine asilimia 18 wamerejea kutoka Misri, Sudan Kusini, na Libya.
Takwimu zinaonesha kuwa, bado kuna wakimbizi wa ndani milioni 8.6, idadi ambayo imepungua kwa asilimia 26 ikilinganishwa na kilele chake. Hata hivyo, Sudan bado ni moja ya nchi zenye idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani duniani.
