
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia uratibu wa masuala ya kibinadamu (OCHA) imesema ukame, mafuriko na vurugu vinaendelea kuwalazimisha watu kukimbia makazi yao na kuongeza msukosuko wa kibinadamu nchini Somalia.
Watu zaidi milioni 3.3, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee, sasa wamepoteza makazi yao kote nchini humo. OCHA ikinukuu takwimu kutoka Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, ilisema kuwa kati ya Januari hadi Septemba pekee, watu zaidi laki 8 walilazimika kukimbia makazi yao, asilimia 70 yao ni kutokana na ukame.
OCHA imeonya kuwa mafuriko yanayohusiana na hali ya El Nino yanaweza kusababisha mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao ifikapo Desemba, na kwamba uhaba mkubwa wa fedha unalazimisha kupunguzwa kwa misaada kwa Somalia.
Idadi ya watu wanaopokea msaada wa chakula ilipungua kutoka milioni 1.1 katika mwezi Januari hadi takriban laki 6 katika mwezi Juni. Maeneo 233 ya kutoa lishe na vituo 380 vya afya pia vimefungwa au kupunguza huduma mwaka huu kutokana na uhaba wa fedha.