Wakili wa Christa Pike amesema kuwa Pike alikuwa na “hasira na kuchanganyikiwa” kwa saa kadhaa baada ya kuzinduka kufuatia jaribio lililoshindikana la Tennessee la kutekeleza hukumu ya kifo. Kwa mujibu wa wakili wake swali la kwanza la Pike lilikuwa, “Niko wapi?”
Wakili wake Randy Spivey alifafanua kuwa Pike, anayeaminika kuwa mtu wa kwanza kunusurika kufa baada ya kudungwa sindano ya kifo wakati wa utekelezaji wa hukumu hiyo, alizinduka kwa namna ya kushangaza wakati mipango ilikuwa ikiandaliwa ya kumtoa kwenye mashine zinazomsaidia kupumua, siku sita tu baada ya kuingizwa katika chumba cha utekelezaji wa hukumu ya kifo.
“Lakini siku ya Jumanne, kila mtu alishangaa kwamba Christa alizinduka na kuanza kuzungumza,” Spivey alisema.
Pike, ambaye alihukumiwa kifo kwa kosa la kumpiga na kumchoma kisu hadi kufa mwanafunzi mwenzake Colleen Slemmer mwaka 1995, anafahamu kilichompata, Spivey alisema.
Hata hivyo, bado kuna maswali mengi kuhusu uwezekano wake wa kupona na iwapo Tennessee itafanya jaribio jingine la kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya Pike, ambaye sasa ana umri wa miaka 50.
