Rais wa China atoa hotuba kwenye Mkutano Usio Rasmi wa 33 wa Viongozi wa APEC

Rais Xi Jinping wa China Alhamisi aliongoza Mkutano Usio Rasmi wa 33 wa Viongozi wa APEC huko Shenzhen, Mkoani Guangdong kusini mwa China, na kutoa hotuba muhimu yenye kichwa “Kujenga Jumuiya ya Asia-Pasifiki, na Kufungua Ukurasa Mpya ya Muujiza wa Asia-Pasifiki.”

Ifuatayo ni nakala kamili ya hotuba:

Wenzangu Wapendwa,

Nimefurahi kuwakaribisha katika jiji zuri la Shenzhen kujadili mustakabali wa ushirikiano wa Asia-Pasifiki.

Kuzinduliwa kwa APEC zaidi ya miaka 30 iliyopita, kulianzisha safari nzuri ya kuelekea kujenga jumuiya ya Asia-Pasifiki. Katika kipindi cha miongo mitatu na zaidi, eneo letu limeshuhudia maendeleo kila siku inayopita, na kuunda muujiza wa ukuaji wa haraka wa uchumi wa Asia-Pasifiki.

Leo, mabadiliko makubwa ambayo hayajaonekana katika karne moja yanaongezeka kwa kasi kote duniani. Ubunifu unaibuka katika sekta za sayansi, teknolojia na viwanda. Ili kukabiliana na fursa na changamoto mpya, ni lazima tuzoee hali halisi mpya, tuchukue hatua mpya, na kuanzisha sura mpya katika ushirikiano wa Asia-Pasifiki. Aidha, lazima tujitahidi kujenga jumuiya ya Asia-Pasifiki yenye sifa ya kushikamana na kusaidiana, kufungua mlango na kuwasiliana, kupanua na kuvumbua, pamoja na maendeleo jumuishi.

— Kujenga jumuiya ya Asia-Pasifiki kunahitaji kushikamana na kusaidiana. Bahari kubwa ya Pasifiki, ambayo hubeba maelfu ya meli na kulea maisha yote, imeunda tabia inayokumbatia mambo yote ya eneo la Asia-Pasifiki — inayofafanuliwa na ujumuishaji na kuishi kwa usawa. Wanachama wa APEC ni kama abiria wanaopanda meli moja. Ili kupitia mawimbi ya Pasifiki, lazima tuungane kama kitu kimoja na kujaliana. Lazima tupanue maslahi yetu ya pamoja, kukabiliana na matatizo na changamoto pamoja, na kujenga kwa uthabiti hisia ya pamoja ya jumuiya.

— Kujenga jumuiya ya Asia-Pasifiki kunahitaji kufungua mlango na kuwasiliana. Ushirikiano wa kufungua mlango ni njia ya lazima ya maendeleo na ustawi wa Asia-Pasifiki. Tunapaswa kudumisha wazo la kikanda la kufungua mlango, kusukuma mbele kwa utaratibu mchakato wa mafungamano ya kiuchumi, na kujenga muundo wa ushirikiano wa kufungua mlango na kufungamana, badala ya kufunga mlango au kutengana. Tunapaswa kutetea biashara na uwekezaji huria na kufungua mlango, kuondoa vikwazo kwenye mtiririko wa mambo, kuhakikisha mzunguko mzuri wa damu ya uchumi, na kupanua nafasi zaidi kwa ukuaji wa uchumi katika Asia-Pasifiki.

— Kujenga jumuiya ya Asia-Pasifiki kunahitaji kupanua na kuvumbua. Uvumbuzi ni nguvu kuu ya maendeleo. Ni muhimu kuhimiza mawasiliano na ushirikiano wa sayansi na teknolojia, kuwezesha uuzaji wa matokeo ya uvumbuzi, na kukuza mazingira ya kufungua mlango, yenye usawa, haki na yasiyobagua kwa ushirikiano. Tunahitaji kuwa na roho ya jitihada, kuongeza jukumu la APEC kama kichocheo, kuhimiza uvumbuzi wa mifumo na mawazo pamoja na mageuzi ya kimuundo, na kuachilia zaidi uhai na uwezo wa uchumi wa eneo letu.

— Kujenga jumuiya ya Asia-Pasifiki kunahitaji maendeleo jumuishi. Kila nchi ikiwa na mahitaji tofauti ya maendeleo, uchumi wa Asia-Pasifiki unajulikana kwa utofauti wetu. Tunapaswa kuendeleza ushirikiano kufuatia hali halisi, kuhakikisha maendeleo yanamnufaisha kila mtu, kuongeza hisia ya kupata ya watu, kujali mambo yanayofurahisha pande mbalimbali, na kulimbikiza mazingira mazuri kwa ajili ya kutimiza malengo ya pamoja ya jumuiya ya Asia-Pasifiki.

Wenzangu Wapendwa,

China ni mtetezi, mhamasishaji na mtangulizi wa ushirikiano wa kiuchumi wa Asia-Pasifiki. Tunapenda kushirikiana na pande zote ili kuunganisha hekima na nguvu katika kujenga nguzo nne muhimu za jumuiya ya Asia-Pasifiki.

Kwanza, tunapaswa kuimarisha nguzo ya uchumi na biashara. Eneo la Biashara Huria la Asia-Pasifiki (FTAAP) ni lengo la pamoja la wanachama wa APEC. Ni muhimu kusukuma mbele kwa hatua thabiti lengo hilo, na kuinua kiwango cha juu zaidi cha kufungua mlango. Jitihada zinapaswa kufanywa ili kuoanisha makubaliano mbalimbali ya kiuchumi na biashara ya kikanda, kuongeza kiwango cha kiurahisi na kidijitali cha biashara na uwekezaji, na kupunguza vizuizi vya biashara na uwekezaji. Pia ni muhimu kuimarisha mazungumzo ya sera kuhusu FTAAP, na kufanya mabadilishano ya uzoefu na ushirikiano wa teknolojia, ili kusaidia pande zote kuongeza uwezo wa kushiriki katika mipango ya kiuchumi na biashara kwa kiwango cha juu.

Pili, tunapaswa kuboresha nguzo ya muunganiko. Muunganiko ni kiungo cha mafungamano wa uchumi wa kikanda. Mwaka 2014, tuliunda kwa pamoja Mpango wa Muunganiko wa APEC. Leo, kuna fursa mpya za muunganiko wa kikanda. Tunapaswa kuimarisha “muunganiko wa hardware” kwa kuboresha mtandao wa miundombinu, na kuhimiza ujenzi wa forodha na usafiri wa teknolojia za akilibandia. Tunapaswa kuimarisha “muunganiko wa software” kwa kuoanisha sera na kanuni, kuimarisha ushirikiano katika malipo ya kuvuka mpaka, na kufanya minyororo ya viwanda na ugavi iwe imara na bila vizuizi. Tunapaswa pia kuimarisha “muunganiko wa moyo” kwa kurahisisha usafiri kwa ajili ya biashara, utalii na madhumuni mengine, na kukuza mawasiliano ya kitamaduni kwa ajili ya maelewano mazuri ya pande zote na uhusiano wa karibu kati ya watu wetu.

Tatu, tunapaswa kujenga nguzo ya uvumbuzi. Uchumi wa kidijitali na akili bandia (AI) ni injini za ukuaji unaoendeshwa na uvumbuzi. Tunapaswa kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya kidijitali, kukamilisha usimamizi na ushirikiano wa kikanda wa data, na kufikia mtiririko wa data wa mipakani wenye ufanisi, urahisi na usalama. Tunapaswa kujenga mfumo unaofungua mlango wa uvumbuzi, kuhimiza matumizi mapana ya AI, na kuhimiza mageuzi na uboreshaji wa sekta za viwanda ili kupata maendeleo yenye sura mpya.

Nne, tunapaswa kuimarisha nguzo ya maendeleo. Ili kukabiliana na changamoto zinazoibuka mara kwa mara duniani, tunapaswa kuimarisha ujenzi wa uwezo, kukuza ushirikiano wa kikanda kuhusu nishati na usalama wa chakula, na kuimarisha mapambano ya kuvuka mipaka dhidi ya ufisadi. Tunapaswa kuhimiza maendeleo ya rasilimali, mazingira na watu kwa uwiano, kuongeza nguvu katika kutumia na kulinda vizuri maliasili, na kupanua ushirikiano wa kijani na wenye utoaji mdogo wa kaboni ili kufikia ukuaji endelevu wa uchumi. Tunapaswa kuunga mkono maboresho ya maisha ya watu na kuwekeza kwa watu, kuanzisha programu za uzee wenye afya, kuhimiza upanuzi wa ajira na ufundi stadi, na kuunga mkono uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake na mawasiliano ya vijana wenye vipaji, ili kuachilia uhai wa vipaji kote Asia-Pasifiki.

China imeweka mizizi yake katika eneo la Asia-Pasifiki na itaendelea kuunga mkono ushirikiano wa eneo hilo. Ninatangaza kwamba China itatoa dola milioni 20 za Kimarekani ili kuunga mkono ushirikiano wa kivitendo wa APEC. Tutaanzisha Kituo cha Utafiti wa Jumuiya ya Asia-Pasifiki mjini Shenzhen, ili kufanya utafiti wa sera na mawasiliano, na kutoa uungaji mkono wa kiakili. Sambamba na mahitaji ya ushirikiano wa Asia-Pasifiki, tutaanzisha taasisi za ushirikiano katika maeneo kama vile teknolojia ya kidijitali, mtiririko wa data wa kuvuka mpaka, nishati safi, na maendeleo ya biashara ndogo na za kati, ili kuchangia ukuaji wa kijani unaotokana na uvumbuzi katika Asia-Pasifiki.

Wenzangu Wapendwa,

Mji wa Shenzhen unajulikana kama Mji wa Roc (jina linalotokana na ndege mkubwa na mwenye nguvu kwenye hadithi). Natumai kwamba kwa juhudi zetu za pamoja, ushirikiano wa Asia-Pasifiki utatanua mabawa yake kama Roc, na kuruka juu na mbali hadi kwenye mustakabali mzuri.

Asanteni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

LEOFM

Maisha TV
Live
Tap to listen live