
Kituo pekee cha nyuklia barani Afrika charejesha uzalishaji wa umeme hadi asilimia 70 baada ya usafi wa dagaa waliokufa
Uzalishaji wa umeme katika kituo pekee cha nishati ya nyuklia nchini Afrika Kusini umeongezeka hadi asilimia 70 baada ya uzalishaji wake kupungua kutokana na malundo ya dagaa waliokufa katika eneo lake la upokeaji wa maji ya bahari.
Shirika la Umeme la Taifa la Afrika Kusini Eskom lilinukuliwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo likisema katika taarifa yake ya Jumatano kwamba “limeongeza uzalishaji salama katika Kitengo cha Koeberg 1 kwa asilimia hadi 70, baada ya awali uzalishaji huo kupunguzwa hadi asilimia 50 kama tahadhari ya kawaida ya usalama.”
Eskom ilisema “Marekebisho yaliyodhibitiwa” yalifuatia pampu ya kupoozea kujizima yenyewe kutokana na mlundiko wa vitu vya baharini vilivyojikusanya katika eneo la upokeaji wa maji ya bahari.
Shirika hilo limeeleza kuwa ongezeko hilo linakuja huku dagaa wakizidi kufa kando ya Pwani ya Kusini-magharibi na Magharibi, ambayo iko chini ya uchunguzi wa mashirika mbalimbali kama ilivyobainishwa katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Wizara ya Misitu, Uvuvi na Mazingira (DFFE).