Umoja wa Mataifa umeonyesha wasiwasi kuhusu kuibuka kwa mapigano mapya nchini Sudan, ukisema mapigano hayo yanawaweka raia katika hatari kubwa na kuwafanya watu wengi zaidi kukimbia makazi yao.
Mkoa wa Blue Nile umerekodi moja ya idadi kubwa ya watu wanaokimbia makazi yao, huku mamlaka za huko zikisema karibu watu 22,000 huenda wamekimbilia eneo la Gisan katika wiki iliyopita huku mapigano yakipamba moto. Vurugu pia zimeshuhudiwa katika mkoa wa Kordofan Kaskazini, ambako shambulio dhidi ya vijiji vinavyozunguka mji wa El Obeid jumamosi iliyopita limeripotiwa kusababisha vifo na majeruhi na watu wengi zaidi kukimbia makazi yao. Mkoani Darfur Magharibi, shambulizi la droni katika soko la mafuta karibu na mpaka na Chad alhamis iliyopita limeripotiwa kusababisha vifo na majeruhi ya raia pamoja na uharibifu wa mali.
Wakati huohuo, mapigano mapya katika miji miwili mkoa wa Kordofan Kusini yamesababisha familia kadhaa kukimbia makazi yao.
Umoja wa Mataifa unazitaka pande zote husika katika mgogoro huo kulinda raia na miundombinu ya kiraia, kuendana na sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kuhakikisha mashirika ya misaada yanatekeleza majukumu yao kwa usalama na uhuru.
