
Umoja wa Afrika (AU) umetoa wito wa kujizuia kabisa na kusitishwa mara moja mapambano kufuatia mvutano unaoongezeka kaskazini mwa Ethiopia.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Umoja huo umesema Mwenyekiti wa Tume ya AU Mahmoud Ali Youssouf alionesha “wasiwasi mkubwa” kuhusu mvutano mpya na kuongezeka kwa mapambano, kufuatia kutwaliwa na kukaliwa kwa viwanja vya ndege katika jimbo la Tigray, pamoja na kuzuiwa kwa wafanyakazi wa serikali kuu na Kikosi cha Ukombozi cha Watu cha Tigray (TPLF) na kuvurugika kwa huduma za anga za raia.
Taarifa hiyo ilisema kwamba, mwenyekiti pia ameonyesha “wasiwasi mkubwa” kuhusu ripoti za kuongezeka kwa uhasama katika sehemu za mikoa ya Tigray na Afar, pamoja na kilichojiri hivi karibuni kuhusiana na kuundwa kwa muungano mpya wa kisiasa na kijeshi ambao unahatarisha kudhoofisha hali zaidi na kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana ya kunyamazisha bunduki tangu 2020.
Ametoa wito wa “kujizuia kwa kiwango cha juu na kusitishwa mara moja kwa vitendo vyote vinavyoweza kuzidisha mivutano,” huku akisisitiza kurejea mara moja kwa mazungumzo ya moja kwa moja ndani ya mfumo wa makubaliano ya Pretoria.